Na; Amiry Juma
   Bismillahi-Rrahmani-Rrahim. 

Anasema Allaah Subhaanahu wa Ta'ala:
}}وَأَقِمِ الصَّلاَةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّـيِّئَاتِ ذَلِكَ ذِكْرَى لِلذَّاكِرِينَ{{
{{Na shika Swalah katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanao kumbuka}} (11:114)
}}وَاسْتَعِينُواْ بِالصَّبْرِ وَالصَّلاَةِ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلاَّ عَلَى الْخَاشِعِينَ{{
{{Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu}} (2:45)
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ameturuzuku zawadi kubwa ambayo thamani yake haina mfano. Lakini kwa ajili ya uzoefu wetu juu yake, mara nyingi hatuipi cheo na heshima inayostahiki zawadi hiyo. Zawadi hiyo yenye thamani kubwa ni Swalah. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alituletea zawadi hii kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) alipopelekwa kwenye mbingu saba katika safari yake ya Mi’raaj. Kama tujuavyo, kwanza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   alipewa Swalah khamsini ambazo zilipunguzwa mpaka tano, zile tunazoziswali sasa; na kwa Ukarimu Wake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) tunapata fadhila ya zile Swalah khamsini vile vile, ilihali tunaswali tano. Subhana Allaah!
Kwa hivyo Swalah yetu, ambayo wengi wetu tunaichukulia kwa wepesi na kuipuuza, ina utukufu wa kukutana kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Inasemekana kuwa yale maneno tunayoyasema katika tashahhud ni kumbukumbu ya mawasiliano yaliyotokea baina ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Mola wake wakati huo wa Mi’raaj. Wa Allaahu A’alam. Kwa hivyo, kila tunapokaa kwenye tashahhud, inatupasa tuwe ni wenye kuzingatia utukufu wa kikao hicho.
Swalah ni mojawapo ya njia kubwa ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametutolea iwe ni hakikisho kuwa tunabaki kwenye njia ya Uislamu ambayo inaongoza kwenye Rehma Yake na Msamaha Wake, na kila zuri duniani na Aakhira. Kwa hakika, Swalah inatuunganisha na Mola wetu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amelinganisha Swalah na mto ambao mtu akioga ndani yake mara tano kwa siku, Hakika mtu huyo hatokuwa mchafu. Hivyo basi, Swalah zetu tano zinazuia kufungika kwa uhusiano baina yetu na Allaah. Kwa hivyo kuswali kwetu, daima kunafuta madhambi madogo yaliyotendeka baina ya kila Swalah. Allaah  (Subhaanahu wa Ta'ala)  Ametufaradhishia Swalah ili daraja zetu zipande, thawabu zetu zizidishwe, na madhambi yetu yadondoke kutoka kwetu, na kwa ajili yake Atutie Peponi na Atuokoe na Moto.
Walakini, Swalah ni kama upanga wenye makali pande zote mbili. Tukiihifadhi, itatupa mwangaza kwenye nyoyo zetu, makaburi yetu, na siku ya Kiama. Itatushuhudia wakati ambao tunahitaji shahidi ili tuokoke na adhabu ya Moto, kama tujuavyo kutoka kwa Yahya ibn Sa'id kwenye Muwatta: “kitendo cha kwanza kutizamwa siku ya Kiama ni Swalah, ikikubaliwa, basi vitendo vyengine vitaangaliwa, lau sio hivyo, basi vitendo vyote pia havitoangaliwa.” Lakini tukiipuza na kuitoa thamani, basi nayo itatoa ushahidi dhidi yetu, wakati ambao tunahitajia shahidi zaidi. Lazima tujihadhari tusiwe miongoni mwa watu wale ambao Allaah  (Subhaanahu wa Ta'ala) anawazungumzia katika Surat Maryam:
}}فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا{{
{{Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha Sala, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kuta malipo ya ubaya}} (19:59)
Na tuzingatie maneno ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) : Jabir amesema, “nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema,
((Kitu ambacho kinasimama baina ya binaadamu na kutokuamini na shirki, ni kuacha Swalah)) [Muslim]
Cheo cha Swalah katika dini ni kama mfano wa mlingoti wa nyumba, ukiwepo, nyumba itakuwa madhubuti na vifaa vyake vyote vitalingana mahali pake. Lakini isipokuweko, basi jengo lote litabomoka na kuwa halina maana.
Kulingana na hayo, ni muhimu kukumbuka kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hatuamrishi kuswali tu, bali Anatuamrisha tuimarishe Swalah, ambapo Mufassirun wote wamekubaliana kuwa kuimarisha Swalah, ina uzito zaidi kuliko kuswali tu rakaa tulizoambiwa. Kuimarisha Swalah ina maanisha shuruti zote za twahara, mahali pa kuswali, nguo, kibla, na mengineyo, yote ni lazima yatimizwe.
'Abdullaah bin Mas'uud amesema, "Yeyote anayetamani kukutana na Allaah  (Subhaanahu wa Ta'ala)  kesho, basi atunze Swalah hizi tano wakati muadhini unapoadhini Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Alimuonesha Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Sunnah zote za muongozo, na kuimarisha Swalah ni moja wapo. Ukiswali nyumbani kwako kama wanao kosa kuswali jama’a, umetupilia mbali Sunnah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) . Na ukitupa Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) , huwezi kuongoka. Mumetuona sisi, na hakuna kati yetu ambao walikosa Swalah ya jama’ah isipokuwa wale wanafiki ambao unafiki wao ulikuwa unajulikana, au wale waliokuwa wagonjwa. Watu walikuwa wanakuja kuswali jama’ah huku wameshikiliwa na watu wawili mpaka wakasimamishwa kwenye safu”.
Share on Google Plus

About Ndoa Katika Uislamu

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment